Mashirika yako wapi?

Baada ya onyesho la filamu jana, tulipoeka barua kutoka mwanamke mmoja anayeishi Uwanja wa Fisi. Alikuwa amemwomba Hadija kumwandikia, mwenyewe hawezi.

"NI MSICHANA AMBAYO ANAOMBA MSAADA KUTOKA KWENU

Anahitaji kusaidiwa awe kama wasichana wengine. Amekaa akafikiria ameona maisha yake yamekuwa magumu. Anaomba mumsaidie awe kama Hadija au Eliza kwani alikuwa anavuta bangi na alikuwa anavuta unga. Na vilevile hana wazazi kwani amevuta unga sasa amechoka. Sasa ameamua kuwa awe msichana mwenye kazi nzuri na maisha mazuri. Anaomba msaidie kadiri ya uwezo wenu kwani ameishia katika mazingira magumu. Amemaua kuacha kuvuta unga na kunywa pombe na vilevile alikuwa ana uza mwili wake. Kwa hiyo akaona maisha yamemshinda, maisha yenyewe ni ya Fisi"

 

Mimi uwezo wa kumsaidia sina. Na katika mashirika sijui hata moja linaloweza kumsaidia kwa sababu ya umri wake – ana miaka zaidi ya 18 ambayo ni mwisho kwa kusaidiwa na Kiwohede. Iliniuma sana jana kuwaona katika sinema, wote wako tayari kubadilika lakini hakuna msaada.

 

Asubuhi hii vijana wamenifuata. Waliniambia kwamba wamefikiria kuweka kikundi cha sanaa, ambacho kitakuwa kinawasaidia wao wenyewe kwa kutunga muziki, maigizo na kucheza mpira. Wakipata pesa kwa kikundi, wangesaidiana kwa kupangisha vyumba kwa kila mmoja baada ya mwengine. Ila wanahitaji msaada kwa kuanzisha hicho kikundi, na hatujui kama kuna shirika lo lote litakalokuwa tayari kuwasaida vijana hawa.